Inatupasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kutupa umri tukiwa katika Uislamu na Iymaan hadi kutufikisha tena kukaribia Mwezi Mtukufu wa Ramadhaan. Na hii ni fursa nyingine Anayotupa Allaah Ta’aala katika maisha yetu kushuhudia mwezi huu na kupata fadhila zake.
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((يَا
أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ
عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ)) (( أَيَّامًا
مَّعْدُودَاتٍ ...
((Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa Swawm, kama waliyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah)) (([Mfunge] siku maalumu za kuhisabika…. [Al-Baqarah: 183-184]
Hii
ni neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)Ambaye Ametujaalia kuwa na
miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au siku bora au masaa bora kuliko
mengine, ambazo thawabu zake za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya
nyakati nyingine. Mfano wake ni kama kunapokuwa na mauzo yaliyopunguzwa bei dukani (sale), ambayo kawaida yake huwekwa kwa muda mdogo tu maalum. Na
muda huu mtu huweza kununua vitu vingi kwa malipo kidogo tu. Hali
kadhalika Ramadhaan, ni mwezi mmoja tu, lakini malipo yake huwa ni mengi
kuliko hata malipo ya miezi yote mingine. Ikiwa mtu atatimiza Swawm
yake inavyopaswa na kufanya mema mengi, na akawa katika Twa'a (utiifu)
kamili na kuomba maghfira, basi hutoka katika mwezi huu akiwa
ameghufuriwa madhambi yake.
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
(( من صام رمضان إيماناً واحتساباً ، غفر له ما تقدم من ذنبه )) أخرجه البخاري ومسلم
((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ramadhaan
ni mwezi ambao tunatimiza Fardhi mojawapo ya Kiislamu. Ni mwezi uliojaa
baraka, kheri na Rahma za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kila Muislamu
inampasa aukaribishe mwezi huu kwa furaha na matumaini kamili.
Zifuatazo ni njia kumi za kujitayarisha kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan na kupata manufaa makubwa pindi utakapotimiza:
1-Du'aa
Anza
kwa kuomba Du'aa kwamba mwezi huu ukufikie wakati umo katika hali ya
siha nzuri na usalama hata uweze kufunga na kufanya ibada zako kwa hamu kubwa na wepesi.
2-Mazoezi katika mwezi wa Sha'abaan
Funga
Sunnah nyingi katika mwezi wa Sha'abaan, soma Qur-aan Juzuu moja kila
siku au chini yake, amka usiku uswali japo Raka'ah mbili, kisha zidisha
kidogo kidogo hadi inapoingia Ramadhaan uwe tayari umeshapata mazoezi
mazuri.
3-Shukurani Na Furaha:
Mshukuru
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kukupa uhai na siha hata uifikie
Ramadhaan nyingine. Imaam An-Nawawy alisema, kwamba shukurani inapasa
kwa kila jambo jema unalojaaliwa kubwa au dogo na vile vile shukurani
inapasa kwa kila jambo baya Analokuepusha nalo Allaah (Subhaanahu wa
Ta’ala). Kwa hivyo fanya 'Sajdatush-Shukr' [Sajda ya kumshukuru Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala)] kwa neema hii tukufu.
Furahia
kukufikia mwezi wa Ramadhaan kama unavyomfurahikia mgeni mpenzi
anapokuja kwako na kumuandalia mazuri yote. Maswahaba (Radhiya Allaahu
‘anhum), walikuwa
wakiamkiana unapoingia mwezi wa Ramadhaan na Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema hivi anapowapa habari nzuri
za mwezi wa Ramadhaan:
((جاءكم شهر مبارك افترض عليكم صيامه تفتح فيه أبواب الجنة وتغلق فيه أبواب الجحيم وتغل فيه الشياطين فيه ليلة خير من ألف شهر من حرم خيرها فقد حرم)) رواه أحمد
((Umekujieni
mwezi wa Ramadhaan, ni mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni
Fardh, milango ya Pepo hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na
mashaytaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi
alfu. Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri] )) [Ahmad]
4-Jipangie wakati na weka maazimio
Ni jambo la kusikitisha kuona watu wengi wanafurahia kuingia mwezi wa Ramadhaan kwa kujiandaa kupanga
mambo ya kidunia badala ya mambo ya Akhera. Wengi hukimbilia kwenda
sokoni kununua nguo za 'Iyd, na kufurahikia vipindi vya Ramadhaan katika
televisheni ambavyo sio vya dini kama 'misalsal' (maonyesho ya sinema yanayoendelea [series]), na pia kuanza kukusanya video za filamu, mipira, na mambo ya kupotezea muda usiku wa Ramadhaan. Pia wengine kunua karata, dhumna, meza ya mchezo wa keram kwa maandalizi ya vipumbazo na vipoteza muda katika mchana wa Ramadhaan ili wasiihisi Swawm au kuupeleka muda haraka kama
wanavyoamini wao. Badala ya kufanya maandalizi ya kununua misahafu ya
ziada, kanda za mawaidha, Qur-aan, kukusanya video za mawaidha na
mafunzo mbalimbali ya Dini, vitabu vya Dini kwa lugha wanayoifahamu kwa
wepesi na kadhalika.
Huu
ni mwezi wa kufanya ibada na fursa ya kujichumia mema mengi yamfaayo
mtu Akhera. Kwa hiyo ndugu Waislamu, tujitahidi kuutumia wakati wetu
wote bila ya kupoteza hata dakika moja, na muhimu sana kujipangia mapema wakati wako kama ifuatavyo:
- Ni bora kujipangia nyakati zote za mwezi mzima vipi utatumia muda wako wa mchana na usiku. Weka maazimio ya dhati kuchukua fursa kamili ya wakati wote wa mwezi huu.
- Weka mpango maalum wa kazi zako hata uweze kuswali kwa wakati kila kipindi, kusoma Qur-aan, kula daku na mengineyo kama tutakavyotaja hapa chini.
- Kama ni mwanafunzi na kama unakuwa ukisoma usiku, lala mapema, kisha uamke uswali Qiyaamul-Llayl na usome masomo yako baada ya hapo.
- Anza mpango wako kwa siku chache na kama unahitaji kurekebisha kuboresha nidhaam yako fanya hivyo uweze kujua nidhaam ipi itakayowafikiana na hali yako.
Nasaha kwa kina Mama na kina Dada:
Fanyeni
maandalizi mapema ya kununua vyakula vya mwezi wa Ramadhaan na
kuviandaa vyenye kuandalika mapema kabla Ramadhaan haijaanza, kama vile;
sambusa, madonge ya chapati, maandazi, maji ya matunda n.k. na kuweka
kwenye mashine ya kugandisha barafu (freezer) au jokofu ili
ikifika Ramadhaan muwe na kazi chache za jikoni na muweze kupata nafasi
kubwa ya kushughulika na Ibaadah mbalimbali kama kusoma Qur-aan,
kusikiliza mawaidha na hata kuhudhuria Darsa za Dini.
5-Tawbah na Maghfirah
Omba Tawbatun-Nasuuha
kwa Mola wako na waombe msamaha wale uliowakosea. Kufanya hivi
kutanufaisha zaidi Swawm na Swalah zako na pia kukupa imani kuwa huna
haki ya mtu.
6-Jifunze Fiqhi ya Swawm
Jifunze
elimu ya mambo yanayohusu Swawm (Fiqhi ya funga), hiyo ni muhimu ili
usije kufanya jambo la kuharibu Swawm yako. Jifunze Swawm kama
aliyokuwa akifunga Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
ndio mfano bora kabisa wa kuufuata.
Swawm haifunguliwi kwa kula na kunywa tu, bali pia ni kujiepusha na maneno mabaya na kufanya mambo mabaya kama kusengenya, kutukana, kugombana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((من لم يدع قول الزور والعمل به والجهل فليس لله حاجة في أن يدع طعامه وشرابه)) البخاري
((Yeyote asiyeacha kusema maneno mabaya? Na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula chake na maji)) [Al-Bukhaariy]
7-Jitayarishe kuchuma mema mengi
- Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa ukarimu, huruma, rahma na mapenzi.
- Panga kabisa na kuweka kiwango fulani cha kutoa Sadaka na kutoa kwa maskini, anzia kwanza kwa ndugu na jamaa.
- Kama inakupasa kutoa Zakah, na umependa iwe katika mwezi wa Ramadhaan fanya hima uitimize Fardhi hii pia.
- Weka 'azma ya kufuturisha kwa kualika ndugu, jamaa, jirani na marafiki kwani kumfuturisha mtu ni thawabu.
((قال صلى الله عليه وسلم : من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألباني
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) ((Atakayemfutarisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy na kasahihisha Imaam Al-Albaaniy]
· Kama unaye jirani asiye Muislamu, mjulishe kuhusu Ramadhaan, faida na Fadhila zake. Hii ni njia na fursa mojawapo ya kufanya da'awah kwa jirani yako.
8-Hitimisha Qur-aan, Hifadhi na jifunzeTarjama
Jipangie
wakati uweze kuhitimisha Qur-aan kwani Ramadhaan ndio mwezi
ulioteremshwa Qur-aan na hii ni Sunnah aliyokuwa akifanya Jibriyl
(‘alayhis-salaam) kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa
sallam) kusoma naye Qur-aan yote:
عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلم أجود الناس، وكان أجود ما يكون في رمضان حين يلقاه جبريل، وكان يلقاه في كل ليلة من رمضان فيدارسه القرآن؛ رواه البخاري
Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhiya-Allaahu ‘anhumaa) kwamba: Mtume
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye
matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora zaidi katika Ramadhaan kwa
sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha
Qur-aan)) [Al-Bukhaariy]
Hadiyth hii inatufundisha yafuatayo:
- Kusoma Qur-aan katika Ramadhaan;
- Kukutana kwa ajili hiyo;
- Kupima hifdh yako ya Qur-aan kwa kukaa na Mwalimu au mwenye elimu nzuri ya Qur-aan kwa kukusikiliza au kukufundisha;
- Kuongeza juhudi za kusoma Qur-aan zaidi katika mwezi wa Ramadhaan:
Katika
muda wa masaa 24 weka saa moja au mbili khaswa iwe ya Qur-aan kusoma na
kujifunza maana ya maneno ya Mola wako uonje ladha ya Qur-aan. AlhamduliLLaahi
Alhidaaya imewaandalia ‘Tarjama Ya Qur-aan Tukufu Neno Kwa Neno’, humo
faida na thawabu nyingi zitapatikana pindi Muislamu atakapojifunza apate
kuelewa maneno ya Mola Wake Mtukufu. Vile
vile jitahidi kujiwekea wakati wa kuhifadhi japo sura ndogo ili ukitoka
katika Ramadhaan uwe una surah zaidi za kusoma katika Swalah zako.
9-Mdhukuru (Mkumbuke) Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Kila Mara
Usiache
ulimi wako na moyo wako kuwa mtupu bila ya kumdhukuru Mola Mtukufu kila
wakati kila mahali. Huku unafanya kazi zako za jikoni, fanya Adkhaar za
Tasbiyh (Subhaana Allaah), Tahliyl (Laa ilaaha illa-Allaah), Tahmiyd
(AlhamduliLLaah), Takbiyr (Allaahu Akbar). Kufanya hivi utajichumia
thawabu maradufu, kwa kutimiza wajib wako na kuongezea kumdhukuru Allaah
(Subhaanahu wa Ta’ala) na juu ya hivyo kuongeza baraka katika kazi
zako:
10-Darsa
Hudhuria
Darsa katika mwezi huu au soma vitabu vya dini, au sikiliza mawaidha.
Jambo hili ni muhimu sana kwani kusikiliza mawaidha ni njia muhimu na
bora kabisa katika kuzidisha imani yako. Kwa hakika unahitaji saa tu
kuweza kutimiza jambo hili muhimu kila siku. Kama huwezi kuhudhuria
msikitini, Alhamdulillah, ALHIDAAYA imejaa mawaidha
mengi ya kusikiliza. Tumia muda wako hata wakati unafanya kazi zako za
nyumba na za jikoni huku unasikiliza mawaidha. Kwa hiyo badala ya
kutazama televisheni na kusikiliza muziki jambo ambalo ni haramu ni bora
utazame na kusikiliza mawaidha ujipatie manufaa, thawabu na kuongeza
elimu yako. Kumbuka kwamba kama vile mwili unavyohitajia chakula, hali
kadhalika Moyo na Nafsi zinahitaji chakula chake nacho ni kumkumbuka
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kila aina ya ukumbusho, na mawaidha na
darsa za dini ni mojawapo ya chakula kizuri kabisa cha kutakasa Moyo na
Nafsi kwa kuzijaza iymaan na mapenzi ya Mola Wako Mtukufu.
Kwa kumalizia, tunasema:
Fungua 'Swafha' (Ukurasa) mpya katika maisha yako
Baada
ya kuweza kuyatimiza hayo yote, bila ya shaka hali yako ya iymaan
imekuwa bora kabisa na utakuwa umejibadilisha na kuwa mtu tofauti na
ulivyo. Kwa hivyo weka maazimio ya kuendelea hata baada ya Ramadhaan
kuwa katika twa'a na ibada, na kuendeleza Qiyaamul-Layl (Swalah za
usiku), kusoma Qur-aan japo kidogo KILA SIKU, na iwe umefungua UKURASA
MPYA wa maisha yako na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Akuendeleze katika hali hii.
Tunachukua
Fursa hii ya kuwaombeeni Ramadhaan yenye baraka na kheri nyingi, tutoke
katika mwezi huu tukiwa tumesafishwa madhambi yetu yote, na wenye
kubeba thawabu nyingi ziwe nzito katika Miyzaan ya Hasanaat (mizani ya
amali njema) Siku ya Qiyaamah.
اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنّأ وَ مِنْكُم صَالح الأّعْماَل
Allaahumma Taqabbal Minnaa wa Minkum Swaalih al-A'amaal. Aamiyn
No comments:
Post a Comment