Vijana
wa Kiislamu! Mwezi wa Ramadhani umetuwadia, hatuna wakati mwengine
tuutarajiao tena na kuutumaini katika kufuzu kwetu usio huu. Balaa zote
za kutuletea maafa hapo kesho (Akhera) tuziepuke na tuwe mbali kabisa
nazo.
Katika mwezi huu hakuna masingizio yoyote, ambayo tunaweza
kujisingizia nayo kama vile kudai kwamba 'O'..... Shetani ametushika
sana! Kwani Mtume (s.a.w.) ametudokezea kwamba, "Mwezi wa Ramadhani
unapoingia, milango yote ya rehema huwa wazi (kuwapokea wanaotaka
kuingia), milango yote ya Jahannam hufungwa na Mashetani wote hutiwa
minyororo ili wasiwahangaishe."
Ajabu kubwa zaidi ni kijana wa Kiislamu kuvaa ushanga, mikufu na
bangili namna wafanyavyo wanawake. Ni hadi lini watajisitahi na kuwa na
haya juu ya haya wayafanyayo?
Ni aibu kubwa kwa vijana wa Kiislamu kuhalifu sheria za dini yao hasa
katika mwezi huu. Kwa kila aliye na uchunguzi, atastaajabu sana kumwona
mtu aliyekuwa mnyenyekevu mchana kutwa, msalihina, kubadili hali hiyo
na kuufanya usiku kuwa sitara ili kumdumishia maasi yake.
Ikiwa hawatajinasihi katika muda huu wa rehma na maghfira wakumbuke kuwa wamo hatarini ya kupoteza imani.
Badala ya kuketi mabarazani kusengenyana na kufitiniana, tunahimizwa
kuingia misikitini na kuendesha ibada mbali mbali na tukisome kitabu cha
Mwenyezi Mungu kwa wingi yaani Qur'ani. Kwani pasi na kufanya hivyo,
tutakuwa tunaupoteza wakati wetu ambao ni wa thamani sana kama
ilivyopokelewa katika kauli za wahenga wa kiarabu kwamba: 'Wakati ni
kama upanga, usipouvunja, (mwishowe) utakukata.'
No comments:
Post a Comment